Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemtaka mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) kuomba msamaha kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa mbunge huyo alipotoka wakati wa uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa kutoa lugha chafu Bungeni.
Amesema kuwa kweli kila mtu huwa ana hasira lakini hakutakiwa kumtolea Spika wa Bunge, Job Ndugai lugha chafu kama ile kwani ni kiongozi wa mhimili mhimu wa Nchi.
“Halima ni Mbunge wangu na tunaheshimiana sana ila kwa hili alilolifanya halikubaliki kwani Spika ni mtu mkubwa sana hata kama Chadema haikutendewa haki, lakini alichokifanya si sahihi nenda kaombe msamaha kwa Spika,”amesema Gwajima.
Aidha, ameongeza kuwa mbunge ni kiongozi wa wananchi ndio waliomchagua akawawakilishe, hivyo anapaswa kujua kutoa lugha chafu bungeni ni kuwadharirisha wapiga kura wake.
Hata hivyo, Gwajima amemtaka Mbunge huyo kuomba msamaha mara moja na asipofanya hivyo atamnyoosha kwani yeye ndio jukumu lake kama kiongozi wa dini.