Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo, Machi 3, 2020 limemshikilia na kumhoji Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwa tuhuma za uchochezi baada ya kusambaza sauti na vipeperushi kwa lugha ya Kisukuma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini humo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, SACP Camillius Wambura amesema kuwa katika jumbe hizo, Gwajima amewahamasisha wasukuma kuunda kikundi cha watu 2,000 kwa lengo la kuwafuatilia na kuwashughulikia watu wanaomtukana Rais John Pombe Magufuli.
Aidha, SACP Camillius ameeleza kuwa Gwajima kupitia ujumbe huo wa sauti amewataka wasukuma matajiri kuungana kwa pamoja kwa lengo la kuwasaidia wasukuma maskini ili kuondoa dhana ya kwamba wasukuma ni maskini na ni washamba.
“Kutokana na jumbe hizo, Jeshi la polisi Kanda ya Dar es Salaam limemhoji Gwajima kutokana na jumbe hizo kuonekana kuhamasisha vitendo vya kikabila, jambo ambalo linaweza kuwagawa Watanzania na kupelekea kuvunjika kwa amani na mshikamano wa nchi utakaotokana na matakaba ya kikabila,” amesema SACP Camillius.
Aidha, ameeleza kuwa baada ya mahojiano hayo Jeshi hilo limemuonya vikali Askofu Gwajima na kumtaka kuacha mara moja vitendo vya kuligawa Taifa kwa kutumia vigezo vya kikabila na pia kwa wote wanaotaka kuligawa Taifa kwa misingi ya ukabila, udini au ukanda.