Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema chanjo ya UVIKO-19 itaanza kutolewa maeneo yasiyokuwa na vituo vya kutolea huduma za afya kupitia huduma ya mkoba ili kufikisha huduma hiyo kwa watu wanaohitaji.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo alipohudhuria mechi ya kirafiki iliyoandaliwa kwa ajili ya uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO-19 kati ya timu viongozi wa dini mbalimbali wanaounda kamati ya amani na timu ya wachambuzi wa habari za michezo, iliyofanyika tarehe 02/09/2021 katika uwanja wa Chamanzi Complex jijini Dar ea Salaam.
Dkt. Gwajima amesema elimu inayoendelea kutolewa imesaidia kuongeza uelewa kwa watu na kuongeza mahitaji ya chanjo hasa kwa watu wanaoishi maeneo yasiyokuwa na vituo vya kutolea huduma za afya.
Naye Mufti Mkuu wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zubeir amesema ni muhimu watu kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 ikiwemo kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabani na maji yanayotiririka au kutumia vipukusi pamoja na kupata chanjo ya UVIKO 19.