Siku moja baada ya wakili wa Askofu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Peter Kibatala kuwaandikia barua Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro amesema hawafanyi kazi kwa kufuata barua ya askofu huyo.
Sirro alithibitisha kupata barua hiyo, lakini akasema kuwa wanaendelea kumtafuta popote pale alipo na wakifahamu watamtia nguvuni.
Sakata la kutafutwa kwa kiongozi huyo linazidi kushika kasi kutokana na sintofahamu ya kubaini alipo, ikiwamo kambi ya muda wa saa saba iliyowekwa na polisi nyumbani kwa Gwajima, ambayo haikuwa na mafanikio wiki iliyopita.
Baada ya sintofahamu ya wiki nzima huku kukiwa na uvumi kuwa yupo nje ya nchi na wengine wakidai yupo nchini, juzi wakili Kibatala aliwasilisha barua Polisi akidai mteja wake yupo nje ya nchi na aliposafiri hakuwa anajua kama anatafutwa na polisi.
Katika barua hiyo Kibatala alisema ameelekezwa na mteja wake kufikisha ujumbe huo na akirejea atajisalimisha polisi kuitikia wito huo.
Jana Kibatala alisisitiza kuwa: “Kwa sasa yupo nje ya nchi akihubiri injili, alisafiri kabla ya kupata taarifa kuwa anatafutwa na polisi ana mashauri katika Mahakama ya Kisutu Julai Mosi, hivyo kabla ya hapo atakuwa amesharejea.”
Lakini Sirro alisema barua hiyo ni kujitetea ambako hakuna maana na wanachofanya wao ni kuendelea kumtafuta badala ya kusubiri ajisalimishe kama ulivyoandikwa waraka huo.
“Suala la kutupa taarifa za kujifanya alikuwa hafahamu kama anatafutwa si kweli, tukifahamu mahali alipo hata sasa hivi tunakwenda kumkamata, hatufanyi kazi kwa kufuata maelekezo yake,” alisema Kamanda Sirro.
Sirro alifafanua kuwa bado wanafuatilia kubaini kama yupo nchini au nje ya nchi, wakitambua ni nje nchi atakamatwa huko huko kwa msaada wa Interpol.
“Hatujafahamu alipo hata huko nje Interpol wapo kuwashughulikia watu kama hawa wanaofanya ukorofi nchini na kukimbilia nje ya nchi wakidhani wanatatua tatizo, kumbe wanaliahirisha,” alisema Sirro

Azam FC Waachana Na Ivo Mapunda
Chadema Wataka Mkutano wa Kumkabidhi Uenyekiti Rais Magufuri Uzuiliwe