Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima amemshauri Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kujiuzulu kutokana na kauli aliyoitoa hivi karibuni iliyotafsiriwa kuwa anapinga hatua za Serikali kukopa kiasi cha Sh. 1.3 trilioni nje ya nchi.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Gwajima amesema kuwa kwakuwa Spika Ndugai anatambua amekosea, ni vyema akajiuzulu kwani akiendelea kutakuwa na mgawanyiko ndani ya Bunge, na kwamba wabunge wataambatana na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Namshauri Spika, hali ni mbaya… wabunge wataambatana na Mama [Rais Samia], atajikuta kwenye Bunge pale atapwaya na sisi tutagawanyika. Namshauri Spika wa Bunge, Job Ndugai ajiuzulu, ili nchi iendelee,” amesema Gwajima.
“Namshauri, hii mambo ya kusema ‘nimekosa mimi, nimekosa sana, Mungu na Watanzania mnisamehe. Sasa kama umekosa basi jiuzulu, haya mambo ya naomba msamaha mpaka lini?”Alihoji na kuendelea, “ukweli una gharama zake, ni bosi wangu nitamkuta bungeni. Lakini namshauri ajiuzulu ili tupate mtu atakayemsaidia Mama.”
Mbunge huyo ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima alisema kuwa kitendo cha Spika Ndugai kutoka hadharani na kupinga hatua ya Rais Samia kuchukua mkopo wa Sh. 1.3 trilioni nje ya nchi, usio na riba, kinaonesha alikuwa na nia ovu kwakuwa zilipitishwa ndani ya Bunge lake na pia alikuwa na nafasi kama Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kumshauri Rais Samia ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho.
“Kwa sababu Mimi ninaanza kuona kwamba kuna nia ovu ambayo ilikuwa pale. Mheshimiwa Ndugai alisema ‘Mama juzijuzi amekopa Sh. 1.3 trilioni. Huwezi ku-personalize mtu, inakopa nchi, inalipa nchi.”
Aliongeza kuwa hoja za Spika Ndugai kudai kuwa deni limefikia Sh. 70 trilioni ni kumtwisha Rais Samia mzigo wa madeni ambayo awamu zilizopita zilikopa kwa ajili ya maendeleo, na yeye anaendelea kwa nafasi yake.
“Wakati Magufuli anaingia madarakani alikuta deni la Sh. trilioni 50.6, wakati anaondoka hadi Machi 2021, wakati Magufuli anafariki ameacha deni la nchi liko Sh. trilioni 56.15. Ni kitu gani kilichofanya Spika Ndugai ambebeshe Mama madeni ya Sh. 70 trilioni wakati ni mkopo wa zamani. Kwanini hakukataa wakati yanapita bungeni, kwanini hakusema kwenye Kamati Kuu ya CCM,” amesema Gwajima.
Mbunge huyo amesema yeye ataendelea kumtetea Rais Samia kwakuwa fedha hizo alizokopa kwa ajili ya maendeleo, zimeifaidisha Tanzania na wananchi wa jimbo lake la Kawe.