SERIKALI imewataka viongozi wa ngazi ya Mikoa na Wilaya Nchini kuhakikisha kwamba wanahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na hatua zote za kujikinga na ugonjwa wa COVID-19 ‘Corona’.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima wakati alipokutana na viongozi wa Mkoa wa Dodoma na kutembelea eneo linalozalisha hewa ya Oksijeni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ili kujionea utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Corona.
Waziri Gwajima amekiri kwamba katika wimbi la kwanza na la pili la ugonjwa wa Corona bidhaa za tiba asili zilisaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo huku akisisitiza kuwa hazijafutwa.
” Niwaombe viongozi wa mikoa yote nchini kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari na hatua za kujikinga, maeneo yenye mikusanyiko kuwepo na watoa elimu ili tuweze kukabiliana na mlipuko huu wa tatu”. Amesema Waziri Gwajima.
Waziri Gwajima ameendelea kuwataka wananchi wavae barakoa, wawe na vitakasa mikono na kuwepo na maji tiririka kwenye maeneo yote yenye mkusanyiko.
Amesema watanzania tayari walishakutana na wimbi la kwanza na lile la pili hivyo wanapaswa kutumia uzoefu walioupata kwenye wimbi lililopita katika kuishi na wimbi la tatu kwa kufuata tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya.
Waziri Gwajima ameongeza kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyosema kuwa Tanzania tayari ina wagonjwa kadhaa hivyo ni vema kila mmoja kuchukua tahadhari za kujilinda yeye na mwenzake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ametoa maagizo kwa Mkuu wa Kikosi cha Barabarani mkoani humo kuhakikisha daladala zote mkoani humo zinapakia abiria kulingana idadi ya viti na hakuna abiria atakayesimama.
RC Mtaka ameagiza pia mameneja wa masoko yote ya Mkoa wa Dodoma kuhakikisha maji tiririka yanakuwepo kwenye masoko yao pamoja na kila mfanyabiashara kuvaa barakoa.
” Niwaombe wananchi wote kujilinda na kulinda wenzake, tuvae barakoa, tuepuke mikusanyiko isiyo na lazima, tubebe vitakasa mikono, tupunguze pia kugusana na kukumbatiana na kwenye nyumba za ibada tuepuke kushikana mikono”. Amesema Mtaka.