Meneja wa Newcastle Utd, Rafa Benitez amedhamiria kumsajili kiungo mchezeshaji, Gylfi Sigurdsson kwa kiasi cha Pauni milioni 15, mwishoni mwa msimu huu, ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kupambana kwenye mshike-mshike wa ligi kuu ya soka nchini England msimu wa mwaka 2017/18.
Rafa amedhamiria kufanya hivyo kutokana na kuwa na muendelezo mzuri kwenye michezo ya ligi daraja la kwanza, ambapo kikosi chake kinaendelea kukaribia mlango wa kupanda daraja.
Kiungo huyo wa klabu ya Swansea amekuwa katika wakati mgumu wa kucheza mara kwa mara chini ya meneja mpya Paul Clement, hali ambayo inampa nafasi Rafa kumsajili kwa urahisi wakati wa majira ya kiangazi.
Chanzo cha habari hii (SunSport) kimeeleza kuwa, Rafa amejipanga kufanya hivyo kutokana na dhumuni la kutotumia kiasi kikubwa cha pesa kwa kuwasaka wachezaji kutoka nje ya England, ambapo uongozi wa The Magpies chini ya mmiliki wake Mike Ashley umejizatiti kubana matumizi katika msimu wa kwanza watakapofanikiwa kucheza ligi kuu.
Hata hivyo Newcastle Utd huenda wakapata upinzani wa hali ya juu katika mpango wa kumsajili Sigurdsson mwenye umri wa miaka 27, kutoka kwenye klabu za West Ham, Everton na Southampton.