Mwenyekiti wa jopo la Majaji wa EJAT 2022 Mkumbwa Ally, amesema upo ukame kwenye habari za uchunguzi kiasi cha kujiuliza iwapo zimepigwa marufuku, kutokana na Habari nyingi zilizowasilishwa kukosa vigezo vya habari za uchunguzi.
Mkumbwa ameyasema hayo wakati akitoa tathmini ya zoezi la kupitia kazi za waandishi wa habari zilizowasilishwa kwa ajili ya kushindana kwenye EJAT 2022, wakati MCT ikitangaza majina ya wateule wa Tuzo hizo katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha.
Amesema, “kuna ukame kwenye habari za uchunguzi….hadi tumejiuliza kwani zimepigwa marufuku? hata zile zilizowasilishwa nyingi zinakosa vigezo vile vya habari za uchunguzi…tunasisitiza uandishi wa habari za uchunguzi zifufuliwe kwa sababu huo ndio uandishi, habari nyingi zinahitaji kufanywa kwa uchunguzi.”
“Kuna vyombo vya habari vichache ambavyo ndio vimeshiriki sana kwenye haya mashindano, hiki sio kitu kibaya kuona chombo fulani kutawala….vipi vyombo vingine? Tunashauri vyombo vingine pia kuleta kazi kushindana kwa sababu inasaidia ninyi kujipima katika umahiri na kutoa kazi ambazo zinaweza kushindanishwa,” amesema Mkumbwa Ally.
Hata hivyo amesema Habari nyingi zimekuwa zikikosa sanaa ya ‘story telling’ na lugha ya uandishi wa habari kutokana na kutekwa nyara na sanaa ama lugha nyingine akitolea mfano siasa ambapo jopo la majaji nane liliongozwa naye na majaji wengine ambao ni Mwanzo Millinga, Peter Nyanje, Mbaraka Islam, Dkt. Egbert Mkoko, Rose Haji na Nasima Haji Chum.