Watu wawili wanaotuhumiwa kwa makosa ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi na gongo, wametoroka wakiwa mikononi mwa polisi katika mahabusu ya mahakama ya wilaya ya Hai.
Kamanda wa polisi mkoa, Emmanuel Lukula amethibitisha watuhumiwa wawili kutoroka wakiwa chini ya uangalizi wa polisi. ” Mmoja anatuhumiwa kwa kosa la kusafirisha mirungi na mwingine kwa kosa la kupatikana na gongo” amesema.
Na kuongeaza ” Katika uchunguzi wa awali tunachunguza mazingira yaliyosababisha kutoroka. Tutachukua hatua stahiki kama tukigundua askari wetu walifanya uzembe kwa namna moja au nyingine, mpaka sasa bado tunaendelea kuchunguza tukio hilo”.
Gazeti la Mwananchi linaeleza kuwa vyanzo vya habari vimeripoti watuhumiwa hao walitoroka ijumaa iliyopita wakati wakiwa mahabusu hiyo ambayo hufungwa kwa kufuli, wakati wakisubiri kupandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yao.
Imeelezwa kuwa tukio limeibua maswali mengi kuhusu namna walivyotoroka mikononi mwa polisi wenye silaha na bila kuvunja kufuli la mahabusu.
Ikumbukwe kuwa hili ni tukio la pili kutokea baada ya julai 27, 2016, mahabusu saba wakiwamo waliokuwa wakituhumiwa kwa wizi wa kutumia silaha na mauji, kuvunja kufuli la chumba cha mahabusu cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kutoweka.