Kwa mara ya Kwanza Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara amemwagia sifa Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Henock Inonga kwa kusema ni moja ya wachezaji wazuri wanaocheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Inonga amekua sehemu ya wachezaji wa Simba SC wanaoanza kikosi cha kwanza na kipenzi cha Kocha Franco Pablo Martin, huku akipewa nafasi ya kuanza katika mchezo dhidi ya Young Africans Jumamosi (April 30).
Manara ametoa sifa hizo mapema leo Jumatano (April 27), alipohojiwa na kituo cha Radio EFM, ambapo amesema hana shaka na Beki huyo kutoka DR Congo, lakini amemtoa kasoro kwa kusema anapenda kucheza na jukwaa.
Manara amesema: “Inonga ni beki mzuri lakini sijui shida yake inakuwa nini pia anapenda kucheza na akili za fans kuliko majukumu yake, kwa beki mzuri hawezi kufanya hivyo.”
“Kuna wakati anafanya jambo ili anufaishe mashabiki hivyo kama ataweza kucheza mpira atafanya vizuri pale akiacha kucheza na jukwaa,”
Inonga alianza kwenye kikosi cha Simba SC kilichopambana na Young Africans katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa sare ya 0-0.
Jumapili (April 24) Beki huyo alikosa mkwaju wa Penati katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, huku akionyesha uwezo mkubwa ndani ya dakika 90.