Baada ya kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Young Africans dhidi ya wachezaji kwa madai hawajitumi uwanjani, Uongozi wa klabu hiyo umeibuka na kutoa ufafanuzi huku ukiwakingia kifua wanaotupiwa lawama hizo.
Young Africans jana Jumatatu (Mei 09) ilipata matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ikiwa sare ya tatu mfululizo kwa timu hiyo baada ya kubanwa na Simba SC kisha Ruvu Shooting.
Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara amesema Uongozi umesikia na kuona malalamiko ya Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo kupitia vyombo vya habari, na umeona kuna haja ya kuweka wazi baadhi ya mambo kwa mujibu wa mazingira wanayoyazunguuka.
Manara amesema hakuna yoyote klabuni hapo anayefurahishwa na kinachoendelea upande wa matokeo walioyapata, zaidi ya kuamini kilichotokea ni matokeo ya mchezo wa soka ambao amesisitiza una matokeo katili.
“Hakuna yoyote hapa klabuni anayefurahishwa na matokeo haya, kinachoendelea kwa sasa ni kuhakikisha tunajipanga ili kuondokana na hali hii kuelekea mchezo wetu dhidi ya Dodoma Jiji FC ambao tutaucheza ugenini.”
“Ndugu zangu mpira ni mchezo wa ajabu sana, na unahitaji uwe na moyo thabit kuushabikia, haipo mechi ambayo tumecheza vizuri zaidi ya jana, Short on Target ni 09, tulipata kona kadhaa, wenzetu wameshindwa kupiga hata Short On Target golini kwetu, ilikua bahati mbaya kwetu na wachezaji wetu walikosa nafasi nyingi sana.”
“Kuna wengine wanalalamika kwa nini Mayele alipewa kugipa Penati, wakati tunaye mchezaji anayepiga Penati Djuma Shaban, jamani Mayele ni Penalt Master amewahi kufunga Penati kabla ya kuja Yanga, haya ingetokea Djuma Shaban Kapiga na amekosa bado mngelaumu kwa nini asingepewa Meyele ili aongeze magoli!”
“Ndugu zangu huu sio wakati wa kulalamikiana, tufanye kiporo chao wameshinda watakabiza alama nane dhidi yetu, alama nane ni michezo mitatu, sisi bado tunaongoza msimamo wa Ligi, tusijipe tabu ambayo haipo kwenye mabega yetu.” amesema Manara.
Licha ya kuambulia matokeo ya sare bila kufungana katika michezo mitatu mfululizo, bado Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 56, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 46.