Msemaji wa klabu ya Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara amesema klabu hiyo haina mpango wa kumuuza Mshambuliaji wake Fiston Kalala Mayele mwishoni mwa msimu huu.
Mayele anatajwa kuwindwa na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kufuatia kuonyesha uwezo mkubwa wa soka tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea AS Vita ya nchini kwao DR Congo.
Manara amesema Mshambuliaji huyo bado ni mchezaji halali wa Young Africans, na hakuna mpango wowote wa kumuuza mwishoni mwa msimu huu kama taarifa zilizoibuka kwenye mitandao ya kijamii majuma mawili yaliyopita.
“Mayele ni mchezaji wa Young Africans na bado ana mkataba wa kuendelea kuitumikia klabu hii, sisi tuwe wakweli tu Young Africans mpaka sasa hatujapata ofa kutoka kwa klabu yoyote ambayo inahitaji mchezaji kutoka Young Africans.
“Siyo tu kwa Mayele hata kwa wachezaji wengine hatujapata barua hiyo na kuhusu Mayele kusajiliwa na timu nyingine kwa hapa nchini mimi naona wanajidanganya na kama walifanikiwa katika misimu iliyopita kumsajili mchezaji Young Africans basi haitawezekana tena.
“Young Africans ya sasa hivi hakuna timu kwa hapa nchini wataweza kusajili mchezaji ambaye Young Africans inamhitaji hiyo ni kwa kuwa wachezaji wengi wana furaha kucheza hapa na wanapata kila kitu,” amesema Manara
Mayele ambaye tayari ameshaifungia Young Africans mabao 10 katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22, ana mkataba hadi mwezi Juni, 2023.