Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo makini na haitaki mzaha katika matumizi ya fedha za umma, zinazoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Majaliwa, ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manyoni na Itigi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida.
“Serikali yenu iko makini na Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza kuwa hataki mzaha na matumizi ya fedha za umma, hakuna atakayebaki salama na hakuna mtumishi atakayeonewa,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema, kuna wizi mkubwa wa mapato ya Serikali kupitia mifumo ya makusanyo kwenye halmashauri nchini ikiwemo na Halmashauri ya Manyoni, hivyo ameagiza kila aliyepewa dhamana ajipange kusimamia makusanyo pamoja na matumizi yake.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Singida Mzalendo Widege kuwahoji wakusanya mapato katika kituo cha mabasi cha Manyoni na katika mnada pamoja na Mkuu wa Idara ya TEHAMA.
“Makusanyo hayasimamiwi vizuri, mfano katika kituo cha mabasi cha Manyoni Bw. Mussa Chacha ambaye si mtumishi ila amepewa kazi ya kukusanya mapato hayo kwa mwezi Juni alipeleka benki shilingi 1,786,000,” amebainisha Majaliwa.
Ameongeza kuwa, “Kikundi cha wakusanya mapato walipewa PoS na mmoja wao alikusanya shilingi milioni 21.8 kwa mwezi na PoS tatu kwa muda wa miezi mitatu zilikusanya shilingi milioni 35, hawa wote lazima watoe maelezo ili hatua zichukuliwe kwa wahusika wote. Fedha hazipelekwi benki na makusanyo yanayopatikana si halisi.”
Kamanda Widege, pia ameagizwa kufuatilia shilingi 11,021,200 zilizoingizwa Julai 12, 2022 benki kupitia namba ya malipo 992310018776 ikiwa ni makusanyo ya kituo hicho baada ya kusikia anafanya ziara katika Halmashauri hiyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Wilaya wahakikishe wanawasimamia Wakuu wa idara katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kupanga muda wa kwenda kuwatembelea wananchi kwenye maeneo yao na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.
“Kila mmoja ahakikishe anatekeleza majukumu yake na kutoa taarifa kwa wananchi juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao, Manyoni hamuendi kwa wananchi, suala la usimamizi ni muhimu sana, Mkuu wa wilaya simamia hili,“ amesisitiza Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoa umepata shilingi bilioni 252 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Dkt. Mahenge amesema, mbali na Mheshimiwa Rais Samia kuidhinisha mkoa kupata fedha hizo za miradi ya maendeleo, pia wamepata ajira za watumishi zaidi ya 800 ambao wanawatumikia wananchi katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya na utawala.