Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa haina upungufu wa chanjo wa aina yeyote kwa watoto hivyo imewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto kuwapatia chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi amesema hayo wakati alipotembelea ghala ya kuhifadhia chanjo lililopo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

“tulikua na upungufu wa aina mbili za chanjo nchini kati ya tisa ambazo tumekuwa tukizitoa lakini, sasa hivi chanjo zote zipo, kwani zimeshawasili hapa nchini na usambazaji unaendelea”, amesema Dkt. Subi

Amesema kuwa, upungufu huo wa chanjo ulitokea baada ya Dunia kukumbwa na janga la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambapo anga zote zilifungwa kwani chanjo husafirishwa kwa mnyororo baridi, kwahiyo huitaji usafiri wa anga.

“Tunamshukuru Rais  John Magufuli kwa kulifungua anga la Tanzania ambapo,  chanjo sasa zimeanza kuingia nchini na hadi sasa mikoa kumi na tatu(13) chanjo hizi zimeshapokelewa kati ya mikoa 26, na mikoa mingine kumi na tatu  ya Tanzania Bara usambazaji unaendelea kupitia Bohari ya Dawa (MSD)”.amesema Dkt. Subi.

Madaktari waliokwama Cuba kurejea
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 22, 2020