Wagonga nyundo wa jijini London (West Ham Utd), wameipiga chini ofa ya klabu ya Olympic Marseille iliyokua imemlenga kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Dimitri Payet.
Olympic Marseille waliwasilisha ofa hiyo wakitaka kumsajili Payet kwa kiasi cha pauni milioni 35 ambacho waliamini kingeweza kuushawishi uongozi wa West Ham Utd ambao kwa sasa upo kwenye harakati za kutafuta suluhu na mchezaji huyo.
Tayari rais wa Olympic Marseille Jacques-Henri Eyraud, alikua ameshaomba kukutana na viongozi wa West Ham Utd ili kupanga mipango ya kukamilisha dili hilo, lakini pia ombi hilo limekataliwa.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, hii ni mara ya pili kwa Olympic Marseille kutuma ofa ya kutaka kumsajili Payet, kwa mara ya kwanza walifanya hivyo mwishoni mwa juma lililopita kwa kuwasilisha ofa ya Pauni milioni 20.
Payet, amekua katika shinikizo la kutaka kuuzwa klabuni hapo, na tayari ameshasusia mazoezi pamoja na kucheza mchezo wa ligi wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Crystal Palace.
Nahodha na kiungo wa West Ham Utd Mark Noble ameonyesha kuguswa na suala hilo, na amefika mbali zaidi kwa kugoma kuzungumza na Payet kwa kigezo cha kuchukizwa na mpango wake wa kushinikiza kuondoka.