Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars imekwama kwenda Kongo- Brazzavile kwenye Michezo ya Afrika kutokana na kutopatiwa usafiri na Serikali.

Malinzi amesema tangu juzi viongozi wa TFF wamekuwa wakishinda ofisi za Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo kufuatilia tiketi, lakini hawajafanikiwa.

“Ni hatari sana iwapo timu hii haitakwenda Kongo-Brazzavile, tunaweza kufungiwa kwenye mashindano yote ya kimataifa, kwa kweli tupo kwenye wakati mgumu,”amesema Malinzi.

Rais huyo wa TFF, amesema wao waliipeleka timu kambini Zanzibar na tangu awali inafahamika suala la kuisafirisha timu kwenda Kongo-Brazzavile ni la Serikali.

“Hii ni sehemu ya Michezo ya Olimpiki na kama unavyojua wanamichezo wote wa Tanzania waliokwenda huko wamesafirishwa na Serikali, hivyo hili nalo ni jukumu lao,”amesema Malinzi.

Michezo ya Afrika (All Africa Games) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho na Twiga Stars itafungua dimba na Ivory Coast Septemba 6, kabla ya kumenyana na Nigeria Septemba 9 na kumaliza mechi za kundi lake kwa kumenyana na wenyeji Kongo-Brazzavile Septemba 12.

Timu mbili kutoka kundi A zitaungana na timu mbili nyingine kutoka kundi B kucheza hatua ya nusu fainali.

Habari zinasema Mawaziri wote wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Dk, Fenela Mukangara na Juma Nkamia wapo ‘bize’ na kampeni za Ubunge na hilo ndilo linasababisha kukwama kwa Twiga Stars.

Rivaldinho Wa Rivaldo Asajiliwa Boavista
Tonny Pulis Amuwekea Kauzibe Saido Berahino