Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, hii leo Novemba 9, 2023 Jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya Wabunge waliotaka kufahamu mpango wa Serikali katika kumaliza changamoto za umeme nchini, amesema hali ya upatikani umeme nchini imeimarika na sasa upungufu wa umeme umebakia 218 MW.
Amesema, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kupunguza upungufu wa umeme nchini kutoka MW 421 hadi MW 218 na hivyo kuimarisha Hali ya Upatikanaji wa Umeme nchini na kwamba Serikali inaendelea na matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme ili kuboresha zaidi Hali ya Upatikanaji wa Umeme nchini. .
Aidha, Naibu Waziri Kapinga ameeleza zaidi kuwa, pamoja na jitihada hizo, Serikali pia imeongeza uzalishaji wa gesi katika visima vya Mnazi Bay, Somanga na Madimba ili kuweza kuongeza gesi ya kuzalisha umeme na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
Amewasisitiza Mameneja wa TANESCO, kuweka utaratibu mzuri wa mgao wa umeme katika Taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi ikiwemo Vituo vya Afya, Ofisi za Serikali, Mashule na n.k ili wananchi waendelee kupata huduma.
Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Christine Ishengoma aliyetaka kufahamu kumalizika kwa tatizo la umeme katika Manispaa ya Morogoro, Mhe. Kapinga, amesema Serikali imefunga mashineumba yenye uwezo wa MVA 120 katika Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msamvu ili kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme kwa mkoa huo.
Kapinga alifafanua kuwa, kazi hiyo ya kufunga mashineumba itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 10.5 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba 2023.
Kuhusu usambazaji wa umeme katika taasisi za elimu, afya, dini, pamoja na visima, Kapinga amesema tayari miradi inaendelea ya kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo wigo wa usambazaji wa umeme huo umeongezwa kutoka kilomita moja hadi mbili ili Taasisi nyingi ziweze kufikiwa.