Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuacha huru Mbunge wa Viti Maalumu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Halima Mdee, baada ya kumkuta hana hatia katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli iliyokuwa inamkabili mahakamani hapo.
Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Februari 25, 2021, na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Simba amesema kuwa upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake watatu umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha mashaka yoyote.
“Baada ya kupitia ushahidi, nimejitosheleza upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka, hivyo mshtakiwa ameachwa huru,” amesema Simba.
Katika kesi hiyo, mbunge huyo wa zamani wa Kawe kupitia Chadema alikuwa akikabiliwa na shtaka moja la kutoa lugha chafu dhidi ya Rais Magufuli , alidaiwa kutenda kosa hilo Julai 3, 2017 katika mkutano wake na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kwa mara kwanza Mdee alipandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Julai 10, 2017.
Alidaiwa kutenda kosa hilo wakati akiwa katika mkutano wake na waandishi wa habari makao makuu ya CHADEMA Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam ambapo alidaiwa kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli.