Wabunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na Ester Bulaya; Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na Kada wa Chama hicho, Kilewo Mwanga leo Machi 13, 2020 wametiwa mbaroni na polisi kufuatia vurugu zilizojitokeza walipokuwa wakifuatilia kuachiwa kwa Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe katika gereza kuu la Segerea.
Viongozi hao wamewekwa chini ya ulinzi kwa madai ya kukiuka amri ya jeshi la polisi iliyowataka kuondoka katika eneo hilo.
Wamekamatwa leo majira ya saa 7 na nusu mchana baada ya polisi kutumia mabomu na kufyatua risasi za kuwatawanya wafuasi wa Chadema.
Aidha, katika vurugu hizo baadhi ya wanachama wa Chadema wamejeruhiwa akiwemo dereva wa bodaboda ambaye inasemekana amevunjika mguu.
Hatua ya kuachiwa huru kwa Freeman Mbowe ni kufuatia kukamilisha kulipia kiasi cha milioni 70 ambazo alikuwa anadaiwa na mahakama kama faini ya hukumu iliyotolewa Machi 10 mwaka huu iliyofikia milioni 350 baada ya kukutwa nahatia ya makosa 12, huku kosa moja likiwa limefutwa.