Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Patrobas Katambi amezitaka Halmashauri na Taasisi za kifedha kutoa mikopo ya vifaa kwa vijana ambao wanakabiliana na changamoto mbalimbali na kutumia fursa zinazowazunguka kujikwamua kiuchumi.
Katambi ametoa wito huo Jijini Dodoma hii leo Oktoba 30, 2019 wakati akifungua mkutano wa Vijana wa East African Community unaojadili fursa na changamoto zinazowakabili vijana na kuwataka kuacha kasumba ya kuajiriwa.
Amesema endapo taasisi hizo zitawakopesha vijana itakua imewasaidia kuacha tabia ya kuahirisha mambo na badala yake watatumia ipasavyo fursa hiyo kwa wakati muafaka ili kufanikisha malengo ya ndoto zao maishani.
“Tuache kasumba za kuajiriwa badala yake tutumie elimu tuliyonayo katika kujiajiri maana zipo fursa mbalimbali zinazotuzunguka ambazo tukizikamata zitasaidia kubadilisha maisha ya ndoto zetu na taasisi za kifedha na Halmashauri zitoe mikopo ya vifaa kufanikisha ndoto za vijana,” amebainisha Katambi.
Aidha ameongeza kuwa Vijana wanatakiwa kutafakari aina ya harakati wanazojishughulisha nazo kuona ni namna gani zinaweza kuwa na matokeo chanya kwao na Taifa zima kwa ujumla.
“Tunasema mikopo ya vifaa maana kwenye suala la ukopaji pesa baadhi ya watu wamekuwa wakishindwa kuirejesha hivyo mbadala huu unaweza saidia walio wengi kufanikiwa kumudu utaratibu wa ukopaji na kutimiza masharti,” amebainisha Katambi.
Awali akiongea katika mkutano huo Mkurugenzi wa Taasisi ya wajibika inayoshughulikia masuala ya vijana John Mlongo amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za uwezeshaji hivyo ni vyema vijana wakaitumia fursa hiyo kujiinua kiuchumi.