Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kuingiza takribani shilingi milioni 160 kwa mwaka baada ya kuingia makubaliano na kampuni ya Uber Tanzania kuhusu uendeshaji wa biashara hiyo ndani ya jiji.
Akizindua ‘stika’ mpya kwa ajili yay a madereva wa Uber, Meya wa Jiji hilo, Isaya Mwita alisema kuwa madereva wote wa Uber watapaswa kununua stika hizo kwa shilingi 80,000 kwa mwaka, fedha zitakazoingia kwenye mfuko wa jiji. Alisema madereva wote wanapaswa kuwa na stika hiyo kabla ya mwezi huu kuisha.
Aidha, Mwita alisema kuwa madereva wote wa Uber watapaswa kuandikisha magari yao na kujipatia leseni ya biashara.
“Tumeona jinsi ambavyo Uber kwa kutumia teknolojia imebadili namna ambavyo watu wanasafiri katika jiji letu. Maelfu ya watu wana njia mpya kujipatia kipato huku wengine zaidi wakipata unafuu wa safari zao,” alisema Mwita.
Meya huyo alisema kuwa kiasi cha fedha kitakachopatikana kutokana na ununuzi wa stika hizo kitatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya jiji.
- Israel yaonya kuipiga Iran, yatungua ndege yake isiyo na rubani
- Video: Diamond akionesha vifaa vya gharama vya Wasafi radio na Wasafi TV
Naye Meneja wa Uber Tanzania, Alfred Msemo aliyezungumza awali alisema kuwa ni jambo jema kuona Uber inaanza kuchangia maendeleo ya jiji la Dar es Salaam kwa kuwataka madereva wake kulipia kwa ajili ya kufanya kazi zao za kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa takwimu, Uber ina madereva 1,500 hadi sasa. Madereva hao sasa watakaguliwa na askari wa usalama barabarani na kutakiwa kuonesha stika ya jiji pamoja na leseni ya udereva wa Uber.