Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imeteketeza Nyavu 115 na Mitumbwi 122 Vyenye thamani ya Tsh, 29,570,000/= Zilizokuwa zikitumiwa na Wavuvi haramu katika eneo la Mbambabay, Ziwa Nyasa kuvulia Samaki na Masalia yake katika ziwa hilo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma, Jimson Mhagama ambapo amesema kuwa zoezi hilo limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani humo, Issabela Chilumba ambaye amewataka wavuvi wote wilayani humo kufuata sheria na taratibu za uvuvi.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa Zoezi hilo ni endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ili kuwabaini na kuwadhibiti Wavuvi haramu ambao wanatumia zana zisizo Rasmi Kuvua samaki pamoja na masalia yake hali ambayo inahatarisha ustawi wa Samaki hao katika Ziwa Nyasa.
“Zoezi hili ni endelevu tumefanya Oparesheni katika eneo la Mbambabay lakini kwakushirikiana na Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tunaendelea kuwasaka watu wote wanaovua samaki kwa kutumia nyavu na mitumbwi Haramu pia tutawachukulia hatua kali za kisheria,”Amesema Mhagama
Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa Wananchi wanaofanya Shughuli za Uvuvi katika Ziwa Nyasa kufuata taratibu na sheria za uvuvi ili ziwa hilo liendelee kuwa salama siku zote kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na Vijavyo.
Hata hivyo, baadhi ya Wananchi walioshuhudia tukio hilo la kuteketeza Nyavu haramu wameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa kuendesha zoezi hilo huku wakitoa wito kwa wavuvi wengine kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali ili ziwa Nyasa liendelee kuwa na Samaki wa kutosha kila wakati kwakuwa Samaki hao ndio mtaji wa Wananchi.