Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amewakumbusha viongozi wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kuwapa vitambulisho vya matibabu bila malipo wazee na wasio na uwezo katika maeneo yao.
Dkt. Dugange ameyasema hayo hii leo tarehe 18 Aprili 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Aloyce John Kamamba aliyetaka kujua ni wazee wangapi wamepewa Bima ya Wazee na waliobaki na ni lini watapewa bima hizo wilayani Kakonko.
Akijibu swali hilo, amesema, “Nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi wote wa Mikoa na Halmashauri kutekeleza maelekezo ya kuwapa vitambulisho vya matibabu bila malipo wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea na wasio na uwezo.”
Aidha ameongeza kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko inatekeleza afua mbalimbali za afya ikiwemo huduma za afya kwa wazee kwa kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea na wasio na uwezo kama ilivyoelekezwa katika sera ya Wazee ya mwaka 2003, sera ya Afya ya mwaka 2007 na mwongozo wa uchangiaji wa huduma za afya nchini.
Alisema kwa mwaka 2022/23, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko iliwatambua wazee wa miaka 60 na kuendelea na wasio na uwezo wapatao 11,524 na kuongeza kuwa, “kati yao wazee 6,084 walipewa vitambulisho vya matibabu bila malipo, wazee 2,000 walikatiwa bima ya mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri.”
Amebainisha kuwa, katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24, Serikali kupitia mapato ya ndani itatenga bajeti kwa ajili ya kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo wazee 3,440 waliobaki katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.