Waziri wa nchi, ofisi ya Rais, tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ameziagiza halmashauri zote nchini kukarabati samani za shule kupitia fedha zinazopelekwa shuleni za programu ya Elimu bila malipo ili kuondoa tatizo la madawati kwenye shule mbalimbali nchini.
Waziri Jafo alitoa agizo hilo kufuatia matokeo ya utafiti wa kampuni ya wazawa ya Mdigiri Logistics kuhusu tathmini ya hali ya vifaa vya ufundishaji na ujifunzaji shule za sekondari mkoa wa Dodoma.
Utafiti huo umebaini hakuna utamaduni wa kufanya marekebisho kwenye vifaa na miundombinu ya shule.
Jafo amesema ni vyema mamlaka za serikali za mitaa kupitia shule zao zinapobaini vifaa na miundombinu yake imeharibika zichukue hatua za kurekebisha na kufanya ukarabati haraka.
” Nielekeze wakurugenzi kutembelea shule katika maeneo yao ambayo yana miundombinu na vifaa vilivyoharibika vinavyohitaji marekebisho kuratibu ukarabati huo kupitia fedha za elimu bila malipo” amesema Jafo.
Aidha amezitaka halmashauri hizo kutumia vikundi vya vijana kufanya ukarabati wa miundombinu ya madarasa, madawati na vifaa vingine vya shule, kuwapa ajira vijana kuboresha mazingira ya elimu katika shule zilizo kwenye mamlaka zao badala ya kusubiri kutenga fedha kutengeneza madawati mapya.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt. Benilith Mahenge amesema utafiti huo umewasaidia kubaini maeneo mbalimbali yenye matatizo na kubainisha watanzania kutokuwa na utaratibu wa kufanya ukarabati.