Kufuatia kusuasua kwa utekelezaji na maendeleo ya Mpango wa Urasimishaji wa Rasilimali na Biashara Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini ambazo zimefikiwa na mpango huo kuwasilisha taarifa rasmi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene katika kikao baina yake na wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa MKURABITA kilichofanyika Ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam.
Simbachawene amesema kuwa TAMISEMI ni mdau muhimu katika Mpango huo wa urasimishaji wa rasilimali hivyo ujio wa kamati hiyo kutaka kushirikiana na Tawala za Mikoa ni jambo jema.
“Binafsi ni muumini wa muda mrefu wa mpango huu wa urasimishaji, niseme tu mmechelewa kuja sehemu husika bila dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi kufanikiwa kwa mpango huu itakuwa ni hadithi, sasa tutaenda pamoja ili kutimiza azma ya mpango huu,”amesema Simbachawene.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA Kapteni Mstaafu wa Jeshi la Ulinzi, John Chiligati amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa Halmashauri zaidi ya 100 nchini mpaka sasa utekelezaji wa mpango huo umezifikia takribani Halmashauri 52 na Miji 9 tu hivyo kasi yake bado hairidhishi.
Hata hivyo, MKURABITA ni miongoni mwa jitihada za Serikali katika kuwezesha jamii kiuchumi. na imeanzishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 2004 kwa lengo la kuwapa nguvu ya kiuchumi wananchi kwa kuwaongezea uwezo wa kumiliki na kufanya biashara katika mfumo rasmi unaozingatia utawala wa sheria. Mpango huu unasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu.