Mwenyekiti wa Kamati za Kudumu ya Bunge na Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa amesema watu wamekuwa hawasemi mazuri ya nchi na badala yake wameshikilia jambo moja la Bandari, kwani ipo nguvu inatumika nyuma ya ya watu wanaopotosha.
Silaa ameyasema hayo wakati akitoa wito kwa Serikali juu ya suala la bandari na kusema hata huko baadae jamii itakuja kuambiwa Bandari imeendelea kuvunja rekodi ya makusanyo, lakini suala hilo bado halitoshi.
Amesema, “wiki iliyopita serikali iliingia mkataba na Uropean Union ya Budget Support, mliona watu wakijadili kuwa fedha hizi zinatoka kwa Mzungu? Juzi tumepitisha bungeni bajeti ya Sh Trilioni 44.39. Lakini watu wameshika jambo moja tu.”
Silaa ameongeza kuwa, “mnaona meli zimepaki zinataka kushusha mzigo. Msidhani kusimama zinapenda, zinasubiri zamu ya kuingia nangani leo mfanyabiashara yoyote tunayemuhudumia akiulizwa, anajibu anaweza kujua jinsi ya kufika bandarini, lakini hawezi kusema lini atashusha mzigo.”
Aidha, amesema suala hilo linatokana na ucheleweshaji na wao kujikuta wakilipa Milioni 60 hadi 90 ya ucheleweshaji huo, na kuongeza gharama kubwa kwa walaji na kwamba hatua hiyo inamshawishi kusema kuna nguvu inatumika nyuma ya hawa wanaopotosha.