Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Hans Pluijm amesema licha ya kuanza na JKU katika mechi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, bado anakiandaa kikosi chake ili kufanya makubwa kwa kutambua michuano hiyo ni migumu na lazima wajipange vyema.
SFG imepangwa na JKU ya Zanzibar katika mechi ya raundi ya kwanza ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu za Tanzania kukutana kwenye michuano ya CAF, lakini Pluijm amesema hiyo haimfanyi kubweteka ndio maana anataka kuwa na kikosi kazi chenye kumbeba Afrika.
Pluijm amesema anaendelea kukifua kikosi hicho ili kujiweka fiti na timu hiyo itashuka uwanjani kwa mara ya kwenye Tamasha la Singida Day litakalofanyika Jumanne ijayo kwa kucheza mechi dhidi ya AS Vita kutoka DR Congo.
“JKU si timu ya kuibeza ni wazuri na tunafahamiana mbinu kwani tulikutana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, hivyo nina kila sababu ya kuandaa timu kimbinu na utimamu lengo ni kuhakikisha tunavuka hatua ya kwanza,” alisema Pluijm na kuongeza;
“Hautakuwa mchezo rahisi tunajiandaa kupambana na nina kikosi kipya, hivyo Jumanne tutakuwa na mchezo mzuri dhidi ya AS Vita ili kufahamu ubora na upungufu yetu.”
Pluijm amesema ni msimu wao wa kwanza wanahitaji kuonyesha ubora ili kuvuka hatua ya awali na hatimaye kutinga hatua ya makundi kitu ambacho amekiri kuwa sio rahisi lakini watapambana.
“Tuna wachezaji wengi wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa hivyo tunaamini itakuwa chachu ya sisi kufanya vyema kwenye mashindano hayo japo sio rahisi bila kujipanga,” amesema Pluijm aliyesisitiza mchezo dhidi ya Vita utatoa picha ya kikosi hicho ili kujua wapi afanye marekebisho.