Mipango ya Mungu, 2010 mpaka 2018 , jifunze kutokata tamaa hata pale unapohisi hakuna msaada wowote katika jambo lako, mtumaini Mwenyezi Mungu kwani ndiye msaada wa mwisho. kubaliana na mapungufu yako kisha yafanyie kazi kusimangwa, kuzaraulika, mateso, shida, magumu yote unayoyapitia yafanye kuwa changamoto kisha ongeza juhudi katika kile ukifanyacho hakika utafanikiwa.
Hayo yameandikwa na msanii wa bongo fleva, Rajabu Ibrahimu maarufu kama Harmonize kupitia ukurasa wake wa Instagram mara baada ya kuposti video yake ya mwaka 2010 akiwa katika shindano la Bongo Star Search na kuimba mbele ya jopo la majaji ambao walipingana na uimbaji wake.
Mbali na Video hiyo Harmonize ambaye kwa sasa ni msanii anayefanya kazi chini ya lebo ya Wasafi Classic Baby, (WCB) ameweka picha nyingine zikionesha mafanikio aliyonayo kupitia muziki wake richa ya kukatishwa tamaa.
Moja ya watu waliotoa maoni katika posti hiyo ni Madam Rita ambaye ndiye alikuwa mtayarishaji wa kipindi hiko cha Bongo Star Search , ameandika amesema ”Mfano wa kuigwa hongera sana”.
Harmonize ni darasa zuri la kujifunzia maisha, kukatishwa tamaa kupo, kikubwa ni kutambua nini unafanya, wakati gani na nini malengo yako, ni vizuri kusimamia yale unayoyaamini kwani ni wachache watakushika mkono wengi watatamani uanguke ili wachekeree na kusema nilijua tu.
Hivyo pambana ukijua wewe ni jeshi la mtu mmoja, acha mafanikio yako yaongee.