Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa Na Michezo Harrison Mwakyembe, amesema hakuna njia ya mkato kwa Tanzania kufanikiwa katika sekta ya michezo zaidi ya kukubali kuwekeza kwa vijana ili kufanikisha lengo la kufanya vyema kitaifa na kimataifa kwa siku za usoni.
Mwakyembe ameyasema hayo alipozungumzana Dar24 mara baada ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Serengeti Boys dhidi ya Ghana ambao ulimalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam jana jioni.
Mwakyembe alisema ni vigumu kwa taifa kama la Tanzania kuwa na ndoto za kufanya vyema kimataifa kwa kutegemea mipango ya kuwatumia wachezaji wakubwa, kwa kuamini wataweza kupambana na mataifa mengine ambao yamejizatiti kwa miaka mingi katika mkakati wa kuwekeza kwa vijana.
“Hatuwezi kufanikiwa kama tutaendelea kuamini mpango wa kuwaamini wachezaji wakubwa tulionao kwa sasa, njia sahihi ambayo mimi kama waziri ninaikubali ni kuwekeza kwa vijana ambao watakua na uwezo mkubwa wa kulitetea taifa lao kwa miaka ya baadae.
“Ipo mifano mingi kwa mataifa makubwa duniani ambayo yanafanya vizuri katika michezo yote, kwa kutegemea mpango wa uwekezaji kwa vijana, unapowaandaa vijana kuna kila sababu ya kuamini miaka mitatu hadi mitano inayofuata kuwa na timu nzuri ambayo itaweza kupambana yoyote Afrika na kwingineko.
“Binafsi ninaunga mkono mpango uliofanywa na TFF wa kuwalea na kuwaendeleza hawa vijana (Serengeti Boys) ambao hii leo kila mmoja wetu anaona fahari kutamba kwa matokeo mazuri tunayoendelea kuyapata, ningependa kuona vyama vingine vya michezo vinaiga mfumo huu, ili kufanikisha hatua ya kuitangaza Tanzania kupitia michezo.” Alisema Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe alikua mmoja wa mashuhuda wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Serengeti Boys na Ghana ambao ulishuhudia dakika kumi za mwisho vijana wa Tanzania wakisawazisha mabao mawili na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare.