Imeripotiwa kuwa Mshambuliaji Harry Kane hatakubali ofa yoyote ya mkataba mpya kutoka kwenye klabu yake ya Tottenham Hotspur na badala yake anachowaza kwa sasa ni kwenda Bayern Munich.
Kane anaingia kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake huko Spurs, ambao wameweka ngumu kumuuza kwa ada isiyofikia Pauni 100 milioni, huku wakiamini watamsainisha mkataba mpya utakaomfanya alipwe mshahara wa Pauni 300,000 kwa juma.
Kwa mujibu wa The Times, Mshambuliaji huyo hana mpango wa kusaini mkataba mpya wa kubaki Spurs kwenye majira haya ya kiangazi, hiyo ikiwa na maana ataondoka bure mwishoni mwa msimu ujao.
Nahodha huyo wa England hatalazimisha kuhama kama alivyofanya mwaka 2021 wakati Manchester City ilipoonyesha kuhitaji saini yake.
Kinachoelezwa ni kwamba kila kitu kipo mezani na Kane yupo tayari kuondoka kwenye dirisha hili kama Spurs wataamua kumuuza ili asiondoke bure mwakani kwa kuwa ataingia kwenye msimu mpya akiwa hajasaini dili jipya.
Na sasa kazi ipo kwa mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy kuamua, amuuze au asubiri kumpoteza bure akitaka kubaki na huduma ya Mshambuliaji huyo kwa msimu huu akiwa na matarajio kwamba atawasaidia kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bayern imeshuhudia ofa zao mbili kwa ajili ya Kane zikikataliwa, huku Mshambuliaji huyo akitarajia kufikisha umri wa miaka 30 juma lijalo. Ofa yao ya pili iliyokataliwa ni Pauni 68.5 milioni pamoja na nyongeza nyingine.