Beki kutoka nchini England Harry Maguire amekasirika na sasa yupo tayari kuachana na Manchester United baada ya kuvuliwa kitambaa cha unahodha kwenye chama hilo la Old Trafford.
Maguire alichukizwa, kukasirishwa na kushangazwa na uamuzi wa kocha Erik ten Hag kumvua unahodha na alimwambia hilo wakiwa mazoezini juzi.
Maguire mwenye umri wa miaka 30, anafahamu nyakati za kubaki Old Trafford zimefika ukomo wakati huu West Ham United, Tottenham Hotspur na Newcastle United zikipiga hesabu kumsajili, huku Chelsea wakiwa tayari kuingia kwenye mbio za kunasa huduma ya beki huyo wa kati.
Maguire, ambaye alisajiliwa kwa Pauni 85 milioni, hakumtaja Ten Hag kwenye posti aliyoandika kwenye mtandao wa kijamiii, alipoandika: “Baada ya kujadiliana na kocha tukiwa mazoezini aliniambia anabadili nahodha.
“Ameeleza sababu zake na hakika binafsi nimehuzunika sana. Nitaendelea kujitolea wakati wote nitakapokuwa nimevaa jezi ya timu hii. Nawashukuru mashabiki wa Manchester United kwa sapoti kipindi chote nilipokuwa nimevaa kitambaa cha unahodha.”
Ripoti zilianza kutoka zaidi ya wiki moja iliyopita kwamba Maguire anavuliwa unahodha, huku Bruno Fernandes akipewa nafasi kubwa ya kutajwa nahodha mpya sambamba na Casemiro.
Na bei ya Maguire kwenye dirisha la Januari ilikuwa Pauni 50 milioni, lakini sasa inaweza kushuka na kufikia Pauni 30 milioni, huku ukiwaweka kando Chelsea wanaomtaka, timu nyingine zinazohitaji saini yake ni Inter Milan, Al-Nassr na Al-Hilal. Mkataba wake umebakiza miaka miwili na analipwa Pauni 200,000 kwa juma.