Klabu ya AC Milan inatajwa kuwa kwenye mpango wa kutaka kumsajili beki wa kati wa Manchester United, Harry Maguire, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Maguire mwenye umri wa miaka 30 hivi karibuni aliweka wazi kuwa ataondoka mwisho wa msimu huu ikiwa ataendelea kutopata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Man United, huduma yake pia inahitajika na West Ham.
Beki huyu aliyesajiliwa na Man Unit ed katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2019 akitokea Leiecester City kwa Euro 87 milioni, mashabiki wengi wa mashetani wekundu wamekuwa hawamuamini na mara kadhaa wamekuwa wakimsema vibaya mitandaoni.
Maguire amesisitiza kwamba ataondoka kwa sababu anahofia nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya England kuelekea michuano ijayo ya Euro 2024.
Mabosi wa AC Milan wanaamini beki huyo anaweza kwenda kusaidia eneo lao la ulinzi licha ya matukio anayofanya kwa sasa akiwa na Man United yanayosababisha timu hiyo iruhusu mabao kwenye michezo kadhaa.