Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa zaidi ya watu 2,400 wameuwa nchini Haiti tangu kuanza kwa mwaka 2023, huku magenge yenye silaha yakiendelea kupambana na Polisi katika jiji la Port-au-Prince huku harufu za maiti zikitanda mtaani na raia wakiomba usaidizi wa usalama kwa mataifa wahisani.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, kati ya Januari 1 hadi Agosti 15, 2023 watu 2,439 wameuawa na wengine 902 wamejeruhiwa, huku wengine 951 wakitekwa na hawajulikani walipo huku Umoja wa Mataifa, ukionya kuwa hali hiyo inazidi kuhatarisha usalama.
Mbali na uwepo wa visa vya mauaji na utekaji, makundi yenye silaha yamekuwa yakiteka magari, kuiba mali na kufanya vitendo vya ubakaji kwa wanawake na wasichana huku wengi wao wakilikimbia jiji hilo.
Tangu kuuliwa kwa Rais wa Taifa hilo, Jovenel Moise mwaka 2021, hali ya usalama ya Haiti imeendelea kuwa mbaya na Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, imekuwa ikiomba hatua za haraka kuchukuliwa.