Uongozi wa klabu ya manispaa ya kinondoni ‘KMC FC’ umeingia mkataba wa mwaka mmoja na nusu na aliyekuwa kocha mkuu wa Lipuli FC ya mjini Iringa Haruna Hererimana raia wa Burundi.
Baada ya bodi ya uongozi wa klabu ya KMC kuridhishwa na Hererimana baada ya kufikia vigezo walivyokuwa wakivihitaji licha ya kuwa na baadhi ya CV mbalimbali za makocha tofauti tofauti waliokuwa wakihitaji nafasi ya kuinoa KMC.
Hererimana anakwenda kuchukua nafasi ya Jackson Mayanja ambaye uongozi uliamua kuachana nae kufuatia matokeo yasiyoridhisha.
Kocha huyo alikuwa akiinoa klabu ya Lipuli tangu kuanza kwa msimu huu akichukua mikoba ya Seleman Matola aliyekuwa ametimkia Polisi Tanzania kabla ya kutua kwenye benchi la Simba SC kama kocha msaidizi.
Kocha Harerimana ametambulishwa kwa wachezaji na tayari ameanza kazi ya kuinoa timu ya KMC kwa ajili ya mashindano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
“Ni kocha ambaye amekidhi vigezo vyote ambavyo tumeweka na uongozi kuamua kuingia naye mkataba. Kupitia yeye, tunaamini timu itafanya vyema na kurejesha ubora wake wa msimu uliopita,” amesema Mwenyekiti wa Bodi ya timu ya KMC, Meya Benjamin Sitta.
Kwa upande wake, Harerimana amesema amekwenda KMC kufanya kazi na kama ilivyo makocha wengi duniani, mafanikio ndiyo malengo makuu.
“Nimekuja kufanya kazi yenye mafanikio, hivyo naomba wachezaji tushirikiane katika kuleta matokeo chanya ya timu na kumaliza ligi katika nafasi nzuri. Nimefurahi kupata uongozi ambao unajali maslahi ya wachezaji na watendaji wa timu,” amesema Harerimana.
Wakati huo ho KMC FC imefikia makubaliano ya kusitisha mikataba na wachezaji watano kutokana na sababu mbalimbali.
Wachezaji hao ni Aaron Lulambo, George Sangija, Rehani Kibingu huku Vitalis Mayanga akiuzwa kwa klabu ya Ndanda FC ya Mtwara.
Wachezaji waliosajiliwa na KMC mpaka sasa ni Janvier Besala Bukungu, Suleyman Ndikumana na Melly Mongolare