Kiungo kutoka nchini Rwanda na klabu ya Young Africans, Haruna Niyonzima amemshauri, Said Khamis Ndemla ambaye anahusishwa na mpango wa kuihama Simba mwishoni mwa msimu huu.
Ndemla anahusishwa na tetesi za kuihama Simba SC, kufuatia kukosa nafasi kwenye kikosi cha mabingwa hao kwa muda mrefu, jambo ambalo linatajwa kwama chanzo cha kudhohofisha uwezo wake.
Niyonzima ambaye amerejea Young Africans baada ya ya kuitumikia Simba kwa misimu miwili, ameeleza kumkubali Ndemla kuwa ni mchezaji mwenye kipaji, lakini anashindwa kuonekana kutokana na uhalisia wa changamoto ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Hata hivyo amemshauri, kuendelea kubaki Simba bila ya kupata nafasi ya kucheza kutaharibu kipaji chake, hivyo ni bora akaondoka na kuangalia mahala pengine ambapo patamuwezesha kuonekana, akicheza soka la ushindani.
“Ndemla ni mchezaji mzuri, unajua Tanzania imejaaliwa wachezaji wenye vipaji vya mpira lakini huwezi kuwa mchezaji mzuri kama haupati nafasi ya kucheza kwenye timu yako lazima kiwango chako kitaporomoka.
“Namshauri atafute changamoto mpya nje ya Simba ili aimarishe kiwango chake kuliko kuendelea kung’ang’ania kwenye timu ambayo hana nafasi ya kucheza,” amesema Noyonzima
Tetesi za usajili ambazo zinamuandama Ndemla mwenye sifa ya kupiga mashuti makali, zimekua zikimuhushishwa kujiunga na Young Africans, pindi mkataba wake na Simba utakapofikia kikomo mwishoni mwa msimu.
Hata hivyo ikitokea Young Africans inamsajili Ndemla, bado atakabiliwa na changamoto ya kupata nafasi mbele ya nahodha Papy Tshishimbi na Feisal Salum.
Lakini mambo yanaweza kubadilika hasa ikitokea kama Tshishimbi ataamua kuondoka, wakati wa dirisha la usajili ambalo litakua wazi mara baada ya msimu huu wa 2019/20 kufikia kikomo.