Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu ya Young Africans Hassan Bumbuli ameijibu KMC FC baada ya klabu hiyo ya Kinondoni Jijini Dar es salaam, kutamba kuondoka na ushindi kesho Jumamosi (Machi 19).
KMC FC itakua mgeni wa Young Africans katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, huku Mkuu wa Idara yao ya Habari na Mawasilino Christina Mwagala akidai tayari wameshazipata Password za wababe hao wa Jangwani.
Bumbuli amesema tambo za KMC FC haziwanyimi usingizi kwa sababu wanafahamu mbinu za kuzima kelele zao, kama ilivyokua kwa klabu nyingine ambazo zilidai zingeweza kuifunga Yooung Africans msimu huu.
“Sijui kama anazo Password zetu, ni vizuri akawa na Password za timu yake ili aweze kuinusuru isishuke daraja, kuliko kuwatunzia Password timu nyingine ambazo huwezi kuzitumia.”
“Kwa hiyo ninamuhakikishia kwamba hawezi kuzitumia Password zetu, tutazitumia wenyewe na tutaifunga KMC FC kesho Jumamosi.” amesema Bumbuli
Kuhusu hali za wachezaji wa Young Africans kuelekeza mchezo huo, Bumbuli amesema hadi sasa wana mejeruhi wawili ambao ni Jesus Moloko na Yacouba Sogne lakini wengine wote wako tayari kukabili KMC FC.
Mchezo wa Duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo mjini Songea Mkoani Ruvuma katika Uwanja wa Majimaji, Young Africans ilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa 2-0, mabao yakifungwa na Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mshambuliaji Fiston Kalala Mayele.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 45 iliyozivuna katika michezo 17 waliyocheza hadi sasa, huku KMC FC ikishika nafasi ya 07 ikiwa na alama 22.