Uongozi wa Young Africans umewahimiza Mashabiki na Wanachama kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa bila kukosa kesho Jumamosi (Machi 19), kwa ajili ya kuipa nguvu timu yao itakapokua na mtihani wa kusaka alama tatu muhimu dhidi ya KMC FC.
Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 45, itakua mwenyeji katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kote.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema Mashabiki na Wanachama wanapaswa kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa bila kukosa, kwa ili kutimiza wajibu wao kwa wachezaji.
“Mashabiki wetu wana kila sababu ya kufika Uwanjani kesho Jumamosi bila kukosa, tunawahitaji sana kwa sababu wamekua msaada mkubwa tangu msimu huu ulipoanza, kufika kwao ni sehemu ya mafanikio ya kikosi chetu ambacho kimedhamiria kuendeleza wimbi la ushindi kama kawaida,”
“Msimu huu Mashabiki wetu tumewapa kipaumbele, kwa sababu ndio salaha kubwa ya maangamizi ya nje ya Uwanja, huku siala ya ndani tukiiacha kwa Wachezaji wetu ambao wamekua wakitufurahisha wakati wote.” amesema Bumbuli
Mchezo huo wa Mzunguuko wa 18 wa Ligi Kuu Tanzania Bara umepoangwa kuanza mishale ya saa moja usiku.
Mchezo wa Duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo mjini Songea Mkoani Ruvuma katika Uwanja wa Majimaji, Young Africans ilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa 2-0, mabao yakifungwa na Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mshambuliaji Fiston Kalala Mayele.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 45 iliyozivuna katika michezo 17 waliyocheza hadi sasa, huku KMC FC ikishika nafasi ya 07 ikiwa na alama 22.