Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Hassan Dalali amefunguka kwa uwazi sababu za kuasisi Tamasha la Simba (Simba Day) ambalo kwa mwaka huu 2021 litafanyika kwa mara ya 12 mfululizo tangu kuasisiswa kwake mwaka 2009.
Dalali chini ya Uongozi wake, aliasisi Tamasha la Simba Day kama sehemu ya kuiwezesha klabu hiyo kupata fedha za kujenga uwanja wake wa mazoezi maeneo ya Bunju, ambapo kwa sasa Uwanja huo unaitwa Mo Simba Arena ambao ndio unatumika kwa mazoezi ya kikosi cha Simba SC kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu na Michuano ya kimataifa.
Dalali amesema anaamini mchango wake ndani ya klabu ya Simba utaendelea kuenziwa na amewataka Mashabiki na Wanachama kuendelea kulidumisha Tamasha la Simba (Sima Day) ambalo kila mwaka limekua likiimarika kwa kuongezewa mambo mazuri.
kama hiyo haitoshi, Dalali akarusha kijembe kwa watani zao wa jadi Young Africans ambao kwa mwaka watatu mfululizo wamefanya tamasha lao la Siku ya Mwananchi ambalo linashabihiana kila kitu na Tamasha la Simba (Simba Day).
Amesema bado anaamini hata upande wa watani zao wa jadi wanaenzi mazuri aliyoyafanya wakati wa utawala wake ndani ya klabu ya Simba kuasisi tamasha la Simba (Simba Day) hivyo hana budi kuwashukuru kwa hilo.