Kiungo wa JKT Tanzania, Hassan Dilunga amesema anasikitika kwa kuwa amepata majeraha tena na atakaa nje zaidi ya miezi miwili.
Dilunga ni kati ya viungo mahiri ambao wamewahi kutikisa kwenye soka la Tanzania akiwa na jezi ya Simba SC, hata hivyo msimu mmoja nyuma alikuwa nje akisumbuliwa na majeraha na alirejea kwenye usajili uliopita na kujiunga na JKT.
Dilunga aliumia kwenye mechi dhidi ya Dodoma jiji wakati timu yake ikipoteza kwa bao 1-0 Uwanja wa Azamn Complex Chamazi Oktoba 30.
Dilunga amesema kuwa wanasubiri uchunguzi zaidi kwa daktari lakini taarifa za awali zinadai kuwa atakaa nje zaidi ya miezi miwili.
Hata hivyo, amesema anasikitika kwa kuwa mguu ambao aliumia kipindi akiwa Simba SC na kukaa nje muda mrefu ndiyo huo huo alioumia sasa akiwa na JKT.
“Naumia sana kwani mguu nilioumia ni uleule nilioumia wakati nikiwa Simba SC, nimeambiwa nitakaa nje kwa zaidi ya miezi miwili naamini nitakaa sawa na kurudi uwanjani, hivi ni changamoto kwa binadamu.” amesema Dilunga ambaye alikuwa panga pangua kwenye kikosi cha Simba SC.