Kiungo Mshambuliaji kutoka Tanzania Hassan Dilunga amesema bado ni mwanafamilia wa Klabu ya Simba SC, licha ya kuwa nje ya kikosi cha Klabu hiyo msimu huu 2022/23.

Dilunga aliachwa kwenye usajili wa klabu hiyo, kufuatia majeraha ya Goti yaliyomuandama tangu msimu uliopita, na sasa ameanza kufanya mazoezi mepesi.

Dilunga aliyejiunga na Simba SC mwaka 2018 akitokea Mtibwa Sugar amesema pamoja na kuwa nje ya usajili wa klabu hiyo, bado anajihisi ni Mwanafanilia ya Msimbazi, kutokana na ukaribu uliopo kati yake na Uongozi wa klabu hiyo.

Amesema anaamini Mashabiki wengi nchini Tanzania walijiuliza kwa nini hakuwa sehemu ya Wachezaji waliosajiliwa Simba SC na kutambulisha wakati wa Tamasha ya Simba Day, lakini ukweli ni kwamba yeye bado ni Mwanafamilia.

vMjWGctfqWhscPrRKTYXS6rfeCxaMQ

“Pamoja na kutokua sehemu ya usajili wa wachezaji msimu huu, niwaeleze kuwa mimi ni Mwanafamilia ya Simba SC, najua wengi walijiuliza maswali kadhaa kuhusu mimi baada ya kutotambulishwa kwenye Tamasha la Simba Day,”

“Niwatoe wasiwasi kuhusu hili, mimi bado ni Mwanafamilia na muda utakapofika kila kitu kitakua wazi kuhusu mustakabali wangu, lakini kwa sasa ninaendelea kujiuguza.” amesema Dulunga

Hata hivyo Mchezaji huyo amekiri hana mkataba na Simba SC, lakini Uongozi wa klabu hiyo umekuwa naye karibu sana, hali ambayo inaendelea kumfariji na kuona bado ni Mwanafamilia.

“Wakati ninapata majeraha, mkataba wangu ulikua umesalia miezi miwili kumalizika, kwa hiyo wakati ninaendelea kujiuguza mkataba ulikua umekwisha, lakini nawashukuru sana viongozi wa Simba SC wameendea kuwa karibu na mimi, ndio maana ninasema mimi bado ni mwanafamilia.” amesema

Dilunga alikua sehemu ya kikosi cha Simba SC kilichopata mafanikio kwa kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara mara nne mfululizo, Kombe la Shirikisho mara mbili na kufika hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2018/19 na 2020/21.

Msimu uliopita Dilunga alifanikiwa kuipeleka Simba SC hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kufunga bao la kufutia machozi dhidi ya Red Arrows ya Zambia iliyoshinda nyumbani 2-1, lakini awali ilipokea kisago cha 3-0 kwenye mchezo uliopigwa jijini Dar es salaam.

Kocha Mtibwa Sugar ataja sababu za kipigo cha 5-0
Kero ya Maji: Serikali yashauriwa kukaa na wadau