Bondia wa ngumi za kulipwa, Hassan Mwakinyo Champez’ ameeleza kutokukubaliana na adhabu ya kufungiwa kwa mwaka mmoja kujihusisha na ndondi na faini ya Sh milioni moja.
Mwakinyo amesema kwa sasa angependa kuwatoa hofu mashabiki wake kwamba wasishtushwe na walichokisikia, kwani ndani ya siku saba alizopewa za kukata rufaa juu ya hilo, atatoa tamko lake rasmi.
“Binafsi nisingependa kuongelea hilo kwa sasa, lakini niwatoe hofu mashabiki wangu kwamba kufungiwa haiwezekani. Mashabiki wasubiri kuona kwamba kwanini nimesema haiwezekani, sio kitu naweza kuzungumza sasa hivi hapa, lakini watapata majibu kabla ya siku saba nilizopewa kuisha.
Juzi Jumanne (Oktoba 10), Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) ilitangaza kumfungia kwa mwaka mmoja bondia huyo kwa kosa la kutopanda ulingoni Septemba 29, mwaka huu.
Pambano hilo lililopangwa kupigwa Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuwania mkanda wa lBA dhidi ya Mnamibia, Julius Indongo, Mwakinyo alikataa kupigana kwa alichoeleza kuwa ni udanganyifu na kukiukwa kwa makubaliano ya msingi na promota wa pambano hilo.
TPBRC ilieleza adhabu hiyo pamoja na faini ya Sh milioni 1 imetokana na Mwakinyo kuchukua uamuzi bila kuheshimu mkataba, kitendo ambacho hakina afya kwa ndondi nchini na kwa ukubwa alionao alipaswa kuonesha mfano kwa mabondia chipukizi, huku alkipewa nafasi ya kukata rufaa ya adhabu hiyo ndani ya siku saba.