Bondia Hassan Mwakinyo amesema atamkubalia Twaha Kassim ‘Kiduku’ kupambana naye iwapo kutakuwa na fedha nyingi zitakazowanufaisha kufanya jambo kubwa la kimaendeleo.
Mashabiki, mabondia na wadau wengi wamekuwa wakitamani mabondia hao wakutane lakini Mwakinyo aliwahi kukataa akisema si wa kiwango chake.
Bondia huyo ametangaza rasmi kuwa anaweza kujibu maombi ya kupambana na Kiduku baada ya kuulizwa maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano wake wa kuzungumzia pambano lake lijalo dhidi ya bondia kutoka Kenya, Reiton Okwiri litakalofanyika kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza Septemba 29, mwaka huu.
Mwakinyo amesema ili kumkubalia Kiduku watu wa Morogoro wanapaswa kuomba dua sana huenda kuna siku atakubali, lakini kwa sharti la kuhakikisha wao wanapata fedha nyingi.
Amesema hata bondia huyo wa Kenya alikuwa akitamani kucheza naye na hatimaye akamkubali na kusema Kiduku na wengine waendelee kuomba kuna siku atawakubalia tu.
Wajiandae kwa sababu haiwezi kuwa pesa ya madafu, ili sote tunufaike. Pambano litakuwa la kihistoria kwao kwa kuwa wataingiza pesa nyingi zaidi kwa hiyo tunataka baada ya pambano tujivunie kufanya kitu kitakachoweka kumbukumbu,” amesema.
Hata hivyo, katika pambano lake la Septemba 29, amesema atawania mkanda wa kimataifa wa IBA na kuwaahidi mashabiki wake wajitokeze kwa wingi kwani hatawaangusha.