Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amewaagiza Wakurugenzi wa Bodi za Mazao kuanza mara moja zoezi la kuwatambua na kuwasajili wakulima wa mazao yote nchini lengo likiwa kuwatambua ili kupanga mipango sahihi yenye kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yote.
Ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao, kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
“Tumepata changamoto kadhaa wakati wa kuwahakiki Wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma na kama Bodi ya Korosho ingekuwa makini kuandaa daftari la wakulima zoezi la uhakiki lingekuwa rahisi, kwa ajili hiyo niliwaagiza Bodi ya Korosho kukamilisha zoezi hili mpaka Mwezi Machi, 2019 na Bodi za Mazao zilizobaki ukiacha Bodi ya Tumbaku ambao wao tayari walishafanya hivyo, kukamilisha Mwezi June, 2019,” amesema Hasunga.
Hata hivyo, Hasunga amesema ili kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya kilimo na kuandaa mipango madhubuti ya kuendeleza mazao yote ni vyema kuwatambua Wakulima wote nchini na kuongeza kuwa Wakulima wa zao la korosho wametoa funzo kubwa kwa Wizara yake kufanya jambo kama hili katika mazao mengine hapa nchini.