Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesaini Hati 8 za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za umeme, gesi, biashara, viwanda na kilimo, utamaduni na sanaa, kumbukumbu na nyaraka, mafunzo katika vyuo vya diplomasia na ushirikiano katika taaluma na teknolojia.
Aidha, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune pia alikutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax aliyemtembelea Ikulu Jijini Algiers, Algeria.
Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano – JPC, kati ya Tanzania na Algeria ulioanza tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 na yalijikita katika kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kirafiki na kidiplomasia, ili kuweza kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya nchi zao.
Aidha, katika kuendelea kuimarisha ushirikiano Waziri Tax pamoja na majukumu mengine, atafanya ufunguzi rasmi wa Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 2 Agosti 2023 Jijini Algiers, huku ufunguzi rasmi wa ofisi za ubalozi huo ni hatua muhimu hasa wakati huu ambapo viongozi hao wamekubaliana kuinua sekta za uchumi ambazo ni pamoja na biashara.
Utiaji saini wa makubaliano hayo, umeshuhudia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria.