Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, imesema kuwa itatoa uamuzi wa kukubali au kukataa maombi ya viongozi wa CHADEMA yaliyotaka kusimamishwa kwa muda kwa usikilizwaji wa kesi yao ifikapo Julai 2 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kusikiliza maombi ya utetezi na mapingamizi ya maombi hayo ya upande wa mashtaka.
Mawakili wa viongozi hao, akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe wamewasilisha maombi ya kusimamishwa kwa muda kwa usikilizaji wa kesi hiyo ya jinai ya mwaka 2018 hadi hapo mahakama itakaposikiliza maombi yao ya marejeo na kutolea uamuzi.
Aidha, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi ameiomba mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo akisema kuwa ni batili.
Hata hivyo, Wakili wa Utetezi Jeremiah Mtobesya amedai kuwa kuwa wanachoomba wateja wake ni haki yao ya msingi na katika mazingira hayo ni haki yao kusikilizwa.
Pamoja na hayo Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja hizo ameeleza kuwa atatoa uamuzi Julai 2, 2018