Kamati ya Utendaji ya Namungo FC imefikia makubaliano ya kuwapa mtihani wa mwisho Kocha Mkuu Hemedi Morocco na Afisa Mtendaji Mkuu wa Omary Kaaya, baada ya kikosi cha klabu hiyo kufanya vibaya kwenye michezo ya Ligi Kuu ya hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Namungo FC Hassan Zidadu amesema kamati yake imekubaliana wawili hao wanapaswa kupambania matokeo chanya kwenye mchezo wa Mzunguuko wasaba wa Ligi Kuu ambao unawakutanisha na Ruvu Shooting.
Zidadu ameweka wazi kuwa wamekuwa na mwenendo ambao hauridhishi katika timu hiyo, hivyo wanaamini kwamba kukiwa na mabadiliko basi wataendelea kufanya kazi na Kocha Mkuu Morocco na Afisa Mtendaji Mkuu Omary Kaaya.
“Kamati ilikutana Jumatatu (Novemba 29) na kujadili mwendo wa timu na kufikia makubaliano hayo na kupewa mechi moja pekee ili kubadili makosa yao,” amesema Zidadu
Namungo FC ilipoteza mchezo wake dhidi ya Tanzania Prisons mwishoni mwa juma lililopita kwa kufungwa mabao 3-1 mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, na kabla ya mchezo huo waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Young Africans.