Uongozi wa klabu ya Yanga umesema unasubiri taarifa ya daktari kuhusu hali ya majeraha inayomkabili mshambuliaji wake , Donald Ngoma ili kuamua kuhusu mkataba wake.
Mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe amekuwa nje ya dimba kwa muda mrefu kutokana na majeraha, mechi yake ya mwisho kuitumikia Yanga ikiwa ni dhidi ya Ndanda FC iliyopigwa katika dimba la Uhuru, Septemba 23,mwaka jana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Hussein Nyika amesema wanachotambua ni kuwa mchezaji huyo bado ana majeraha, lakini pia wanasikitika kukosa huduma yake uwanjani kwani analipwa mshahara kwa ajili ya kuitumikia timu.
Amesema daktari wa timu hiyo anamfanyia vipimo vya mwisho na baada ya siku mbili kuanzia leo, watapata majibu ambayo yatawaongoza katika uamuzi watakaouchukua.