Klabu ya Tabora United iko katika mazungumzo ya mwisho ya kumrejesha aliyekuwa kiungo wa timu hiyo Mkongomani, Papy Tshishimbi aliyekuwa Ihefu FC, huku Kocha Mkuu, Goran Kopunovic akiachiwa msala wa staa huyo.
Tshishimbi aliyewahi kuichezea timu hiyo wakati ikiwa Ligi ya Championship hakupata nafasi ya kucheza akiwa na Ihefu FC tangu Januari 2023, baada ya kusumbuliwa na matatizo ya mara kwa mara ya goti.
“Usajili wake utategemea na mapendekezo ya kocha Goran ndani ya kikosi chetu hivyo kama ataona anafaa kuitumikia timu yetu basi tutamsajili kwa ajili ya msimu ujao,” zimeeleza taarifa kutoka Tabora United
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Adam Simba amesema sababu kubwa ya kutokamilisha usajili ni kutokana na umakini mkubwa wa kutafuta wachezaji ambao watakuwa ni chachu ya mafanikio kwao.
“Wapo wachezaji tunaoendelea na mazungumzo nao na tukikamilisha tutaweka wazi kwa sababu bado siku ni nyingi na tunahitaji kufanya usajili makini ili kuleta ushindani msimu ujao,” amesema