Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema Waganda ndio wenye hatma ya kuchagua ni nani anafaa kuwa rais wao na si vinginevyo kama watu wanavyofikiri.
Museveni ameyasema hayo kufuatia kauli aliyoitoa mwanae Muhoozi Kainerugaba (48), kupitia chapisho aliloandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa atagombea Urais wa Uganda.
Amesema, “Tupo katika mjadala ili Muhoozi ajiondoe kwenye mtandao wa Twitter, ingawa Twitter sio tatizo ila tatizo ni kile anachoandika kwenye Twitter.”
Museveni ameongeza kuwa, Rais huwa hachaguliwi kwenye Twitter hivyo kama Waganda wataona Muhoozi anafaa kuwa Rais wao basi watamchagua kwasababu amekuwa ni Afisa wa jeshi mzuri hivyo maswala ya Twitter hayawezi kumpa ubaya.
Kuhusu kufanya maamuzi ya mrithi wa kiti chake, Museveni amesema Chama chake Cha NRM ndiyo chenye hatma ya ni nani apitishwe kugombea kiti Cha Urais na kwamba, yeye hana maamuzi yoyote kwa mujibu wa utaratibu.
Hata hivyo, Kainerugaba, amesema, bado ataweza kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kwamba kinachotakiwa ni kujizuia kutoa maoni yake kuhusu mambo yenye utata.