Kutambuliwa kwa kazi nzuri uliyofanya ni muhimu katika maendelep ya kazi yako. Kuna wakati Bosi wako akataka kukuzawadia kutokana na kazi zako na ungependa kutambuliwa na wenzako pia.
Hivyo unahitaji kuhakikisha kazi zote ngumu ulizofanya zinatambuliwa vizuri. Kwa bahati mbaya, wakati mwingine kazi yako inaweza isitambuliwe kwa sababu tu ya mwenzako, ikiwa ni kwa makusudi au bahati mbaya akachukua sifa kutokana na kazi yako. Hii inaweza kuathiri utendaji wako na hata kudumaza maendeleo yako ya kazi.
Ikitokea mfanyakazi mwenzako anajisifia na kuchukua sifa kwa kazi uliyofanya, hizi ni namna ya kukabiliana na hali hii:
1. Ongelea Hili Mapema Iwezekanavyo
Firia mko katika kikao na wafanyakazi wenzako, kisha mfanyakazi mwenzako mmoja akawasilisha mawazo ya kazi mliyofanya pamoja huku akijinadi kuwa ni yake. Kisha kila mtu anampigia makofi na kumsifia kwa kazi yake. Utafanya nini? Hakikikisha kwamba kila mtu katika kikao anaelewa mchango wako katika kazi hiyo. Mwache kwanza amalize malezo yake kabla ya kuelezea mawazo yako.
Ikiwa kuna ulazima wa kuingilia kati, hakikisha unadhibiti hisia zako na toa maelezo yako kitaalamu. Usizungushe maelezo na elezea kwa usahihi. Hata hivyo, kuwa makini wakati wa kuelezea wasiwasi wako juu ya kazi hiyo. Usilaumu moja kwa moja kuwa wamekuibia mawazo yako. Badala yake, fanya kama unauliza swali na kutaka ufafanuzi zaidi wa kwa nini hilo limetokea.
2. Ongea nae Baada ya Kikao Mkiwa Wawili na Kwa Upole
Inawezekana mfanyakazi mwenzako akawa amechukua sifa za kazi zako bila kudhamiria. Hivyo badala ya kumtuhumu moja kwa moja, fanya madai yako kwa kama maswali. Kwa mfano, unaweza kumuuliza swali kama "Vipi, umeweza kuelezea pointi zote kama tulivyojadili mwanzoni? Mbona nilisikia unatumia ‘Nili.., Nime..’ nadala ya ‘Tuli.., Tume…, wakati tumefanya kazi watu wawili?
Ulifanyahivyo kwa makusudi? Hii itasaidia kumpa mfanyakazi mwenzako fursa ya kutambua kosa lake, ikiwaalifanya hivyo bila kutambua. Mkimaliza, malizeni tofauti zenu na mweleze kuwa hakuna hisia mbaya kati yeni. Endeleeni kupiga kazi.
3. Futeni Tofauti Zenu
Ikiwa mfanyakazi mwenzako anakubali na anaelewa kuwa amefanya makosa, daima kuna nafasi ya kuweka mambo sawa. Mnaweza kujadili njia bora ya kuweka mambo sawa kwa meneja wenu na wale waliohusika. Mfano, anaweza kuchagua kuandika barua pepe kwenda kwa meneja na timu nzima, kuelezea na kukushukuru wazi kwa mchango wako ili kila mtu aweze kuelewa ushiriki wako katika mradi huo.
4. Omba Ushauri Kwa Wafanyakazi Waandamizi
Ikiwa mmeshindwa kufikia muafaka na kutatua hali hiyo na mwenzako, huenda ukahitaji kuonana na wafanyakazi waandamizi kwa msaada zaidi. Inawezekana waliwahi kukutana na suala kama hiyo kabla na wakawa na uwezo mkubwa zaidi wa kutatua hili kutokana na uzoefu. Hata hivyo, kuwa mwangalifu usije kuonekana kama unanung'unika na badala yake fanya kama ni jitihada za kujenga uhusiano mzuri wa kufanya kazi. Ikiwa hali hiyo itaendelea, huenda ukahitaji kulifikisha hili kwa Bosi wenu na umwache alitatue hili.
5. Kuwa Makini Lisijirudie Tena
Katika siku zijazo, jitahidi kuzuia hili kutokea tena. Tumia fursa zote zinazofaa katika ofisi ili kuchangia mawazo yako na kuonyesha ushiriki wako katika miradi tofauti. Zaidi ya hayo, hakikisha kwamba unamweka bosi wako katika nakala zote za barua pepe za kazi na miradi unayoifanyia kazi.
Pia, hakikisha kuwa, hata kipindi cha chemsha bongo kutafuta njia rahisi ya kufanya kazi fulani, unachangia vyema mawazo yako ili kila mtu ajue kuwa wazo fulani lilianzia kwako. Ingawa si lazima kusifiwa kwa kwa kila kazi unayofanya, kutambuliwa kwa mchango wako kwenye kazi ni muhimu. Hivyo, ikiwa mnafanya kazi ya kikundi, hakikisha kwamba inajulikana wazi kila mtu anafanya kipengele gani mapema ili kuepuka mkanganyiko mwisho wa kazi.